Mkurugenzi wa Idara ya Usajili wa Vitambulisho vya Mzanzibari
Mkazi, Mohamed Juma Ame, akionyesha vitambulisho 25,673 vinavyotakiwa
kuharibiwa baada ya wahusika kushindwa kujitokeza kuchukua tangu mwaka
2010 katika Kisiwa cha Pemba.
Mkurugenzi wa Idara ya Usajili na Vitambulisho vya Mzanzibari Mkazi, Mohamed Juma Ame, alisema kwa mujibu wa sheria, vitambulisho hivyo vitalazimika kuharibiwa kutokana na wahusika kushindwa kujitokeza na kuvichukua.
“Sheria inatuelekeza kuwa ndani ya miaka mitatu, watu wote waliosajiliwa wanapaswa kuchukua vitambulisho vyao, na wale watakaoshindwa kuvichukua, vinapaswa kuharibiwa,” alifafanua.
Alisema uhakiki uliofanyika kisiwani Pemba na kuwashirikisha wabunge, wawakilishi na madiwani, inaonekana kuna vitambulisho vingi havijachukuliwa na wahusika baadhi yao ni walimu na wananchi wa kawaida katika wilaya nne za kisiwani humo.
Alizitaja wilaya na idadi ya vitambulisho ambavyo havijachukuliwa katika mabno kuwa ni Wete (7,498), Wilaya ya Micheweni (5,655), Wilaya ya Chakechake (6,333) na Wilaya ya Mkoani (6,187).
Alisema watu hao wamesababisha hasara kubwa ingawa serikali imelazimika kufanya kikao na viongozi wa majimbo wakiwamo wabunge, wawakilishi na madiwani ili wasaidie kuwapata watu hao kabla ya vitambulisho hivyo kuharibiwa mwaka huu.
Alisema kikao kilichofanyika Febuari, mwaka huu cha viongozi waandamizi na wanasiasa kisiwani Pemba, kilikubalika kutayarisha orodha ya majina ya watu ambao hawajachukua vitambulisho vyao ili wasakwe katika kila shehia kwa kushirikiana na viongozi wa maeneo hayo.
“Kuna wengine picha zao zinafahamika wakiwamo walimu, tunashindwa kufahamu kwa nini wazito kuja kuchukua vitambulisho vyao,” alisema.
Hata hivyo, alisema kuna baadhi ya watu walifanya jaribio la kutaka kuchukua vitambulisho wakati hawana sifa, kwa kughushi vyeti vya kuzaliwa, jambo ambalo ni kinyume cha sheria, huku mfumo wa kudhibiti nyaraka bandia, ulifanikiwa kuwanasa na kuwafikishwa katika vyombo vya sheria kisiwani humo.
Kuhusu malalamiko yanayotolewa na baadhi ya wanasiasa Zanzibar kwamba wapo watoto chini ya umri wa miaka 18 wanasajiliwa, Mkurugenzi huyo alisema malalamiko hayo hayana msingi wowote kwa vile idara hiyo inatekeleza taratibu zake kwa mujibu wa Katiba na sheria.
Alisema kwa mujibu wa sheria, hakuna mtu yeyote anayeruhusiwa kusajiliwa bila kuonyesha cheti chake cha kuzaliwa na kuwataka wananchi wenye sifa kujitokeza na kusajiliwa katika ofisi za idara hiyo zilizopo katika visiwa vya Unguja na Pemba.
Hivi karibuni, Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, alisema kuna watu wengi wanalalamika hawajapatiwa vitambulisho hivyo kutokana na urasimu unaofanywa na masheha na kuwanyima haki ya huduma mbalimbali kupitia vitambulisho hivyo.
Hata hivyo, alisema chama chake kimeridhika na uamuzi wa serikali kuwasaka watu nyumba kwa nyumba ambao wamesajiliwa na kushindwa kujitokeza kuchukua, mpango aliosema utasadia kupata ikweli katika suala hilo.
CHANZO: NIPASHE
Post a Comment