Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein
ameuagiza Mkoa wa kaskazini Unguja kufanya jitihada za makusudi
kuhakisha kuwa Vijiji vya Kidagoni na Matetema vinafikiwa na huduma za
ulazima kama vile Elimu ,Afya Maji na barabara.
Vijiji
hivyo vimekosa huduma hizo muhimu toka kutokea kwa Mapinduzi Matukufu
ya Zanzibar mwaka 1964 ambapo hivi karibuni wakaazi wake waliweza
kujenga Skuli ya Msingi kuanzia Darasa la kwanza hadi la Tano.
Rais
Shein ametoa agizo hilo kwa Watendaji wa Mkoa huo katika Ukumbi wa
Hoteli ya Sea cliff , Michungwa Miwili wakati alipokuwa akifanya
majumuisho ya ziara yake kwa Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Amesema
Viongozi wa Mkoa huo wanapaswa kuvijengea uwezo Vijiji hivyo katika
mambo ya msingi ili viweze kufaidika na huduma ambazo Wizara na Serikali
husika imekuwa ikizitoa kwa Wananchi wake.
“Kwa
vile Wanavijiji wenyewe sasa wameshaamua kuwa karibu na maendeleo basi
ni vyema Serikali nayo ikaonesha jitihada zake kwa kuwaendeleza” Alisema
Rais Shein.
Aidha
Dkt Shein aliwataka Viongozi wa Mkoa huo kushirikiana na Wizara ya
Aridhi Maji na Nishati ili kuimaliza migogoro ya ardhi ambayo imekuwa
sugu kumalizika katika Mkoa huo.
Dkt
Shein pia aliitaka Serikali ya Mkoa huo kukomesha matukio ya
unyanyasaji wa kijinsia yaliyoshamiri sambamba na kufanya taratibu za
kuondoa matuta yasio na ulazima barabarani kwa kushirikia na Wizara ya
Miundombinu.
Wakati
huo huo Dkt. Shein aliulaumu uongozi wa Mkoa huo kwa kushindwa
kutekeleza maagizo aliyoyatoa mwaka jana ya kupanda Minazi na Mikarafuu
lakini katika taarifa yao ya Mkoa haikueleza utekelezaji wa hilo.
Aidha
Uongozi huo haukueleza hali ya Maambukizi ya Virusi vya Ukimwi,
Matatizo ya udhalilishaji wa kijinsia, madawa ya kulevya, Sekta ya
mifugo na hali ya Usalama barabarani.
Katika
hatua nyingine Rais Shein aliupongeza Mkoa huo kwa kufanikiwa kulima
hekta 780 za Mpunga na kuvuka lengo lililopangwa ambapo Mkoa wa
Kaskazini ulilima jumla ya Asilimia 102 ya mashamba.
Kwa
upande wake Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali ambaye pia ni
Mwakilishi wa Jimbo la Donge Ali Juma Shamuhuna akitoa neno la shukurani
kwa niaba ya Watu wa Mkoa huo alimshukuru Rais kwa kuwatembelea na
kuahidi kutekeleza maagizo yote yaliyotolewa.
Katika
ziara hiyo Rais Shein alitembelea Miradi mbalimbali ya Maendeleo
ikiwemo Kilimo, Afya, Elimu na Miundombinu ambapo baada ya Ziara hiyo
Dkt Shein ataendelea na Ziara yake Katika Kisiwa cha Pemba.
MWISHO.
IMETOLEWA NA HABARI Maelezo Zanzibar 14/3/2013
Post a Comment