Polisi kortini kwa wizi wa mil. 150/-

Thursday, 14 March 20130 comments



ASKARI watano wa Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam jana walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na kosa la wizi wa sh milioni 150 mali ya Mire Artan Ismail.
 
Mbele ya Hakimu Mkazi Emilius Mchauro, Wakili Mwandamizi wa Serikali, Bernard Kongola, aliwataja washitakiwa hao kuwa ni Sajenti Duncan Mwasabila (43) mkazi wa Kiwalani, Koplo Geofrey (39) mkazi wa Mbezi Luis, Koplo Rajab Nkurukwa (46) mkazi wa Buguruni, Koplo Kawanani Humphrey (34) mkazi wa Kijitonyama na Koplo Kelvin Mohamed (49) mkazi wa Gongo la Mboto, wote wa jijini Dar es Salaam.

Wakili Kongola alidai kuwa Desemba 18 mwaka jana katika eneo la Kariakoo Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam, washitakiwa walitenda kosa hilo  na akadai upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na washitakiwa wote walikanusha shitaka hilo.

Hakimu Mchauro alisema washitakiwa walikuwa na haki ya kupewa dhamana na kumtaka kila mmoja kuwa na wadhamini wawili wanaofanya kazi katika ofisi zinazotambuliwa na sh milioni tano kimaandishi.
Mbali na kuwa na wadhamini, washitakiwa walitakiwa kila mmoja kulipa fedha taslimu sh milioni 15 au mali isiyohamishika yenye thamani ya kiasi hicho cha fedha.


Hata hivyo ni washitakiwa wanne tu kati ya watano ndio walitimiza masharti ya dhamana jana na mshitakiwa Mohamed alishindwa kutimiza masharti hayo, hivyo hakimu kuamuru apelekwe gerezani na arejeshwe leo mahakamani hapo kwa ajili ya kutimiza masharti hayo ya dhamana. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Machi 27 mwaka huu itakapokuja kwa ajili ya kutajwa.

CHANZO TANZANIA DAIMA
Share this article :

Post a Comment

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. Zanzibar News - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger