Shirika la Umeme Zanzibar { ZECO } limeagizwa kuufanyia matengenezo makubwa mfumo wa umeme uliopo katika Kijiji cha Michamvi Kilichopo Wilaya ya Kati ambao uko katika mazingira ya hatari kwa wananchi wapitao kwenye maeneo hayo.
Agizo hilo limetolewa na Makamau wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipofanya ziara ya ghafla katika eneo hilo kuangalia waya za umeme zilizoanguka chini ya ardhi pembezoni mwa Hoteli za Utalii Beach Resort na Kilele Beach Vila Michamvi kufuatia nguzo zake kung’oka kwa zaidi ya miaka mitatu sasa.
Balozi Seif alifanya ziara hiyo kufuatia malalamiko ya Wananchi wa Michamvi waliyoyatoa kupitia Kipindi maalum cha Mawio kinachotolewa na Shirika la Utangazaji Zanzibar { ZBC } kila siku asubuhi.
Balozi Seif akiambatana na Wakuu wa Wilaya za Kati na Kusini alisema wahandisi wa Shirika la umeme wanapaswa kufanya marekebisho hayo haraka iwezekanavyo ili kukinga athari zinayoweza kuleta maafa hapo baadaye.
Alisema haipendezi kuona watendaji hao wanaripotiwa matukio mbali mbali ya hitilafu za umeme katika maeneo mbali mbali lakini utekelezaji wa hatua hizo huchukuwa muda mrefu jambo ambalo linavunja moyo wale wanaotoa taarifa hizo.
Balozi Seif alifahamisha kwamba uchelewaji wa hatua hizo husababisha baadhi ya watu kujiungia wenyewe huduma hizo bila ya kuzingatia athari za baadaye pamoja na wengine kutumia fursa hiyo kwa kufanya wizi na hujuma zinazopelekea kulitia hasara shirika hilo.
“ Kumekuwa na uchelewaji wa kuchukuliwa hatua kunakofanywa na wahandishi wa Shirika la Umeme wakati inapotokea hitilafu ya kiufundi. Na hili hata mimi mwenyewe nimelishuhudia katika makazi yangu ninayoishi Mazizini. Hebu jitahidini kupunguza malalamiko ya wananchi mnaowapatia huduma za Umeme”. Balozi Seif aliwasa wahandisi hao.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kati Nd. Vuai Mwinyi alimueleza Balozi Seif kwamba tatizo hilo amelirithi kwa Mkuu wa Wilaya aliyemtangulia na kuchukuwa hatua za kuwaandikia Barua ya kuwakumbusha watendaji hao.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif pia alipata fursa ya kuangalia Waya nyengine zilizoanguka za umeme mkubwa katika njia inayokwenda Wilaya ya Kusini ambayo ni miongoni mwa mradi wa umeme uliofadhiliwa na Serikali ya Norway kupitia Shirika lake la Misaada la Norad .
Kwa mujibu wa taarifa za wakaazi wa Kijiji cha Pete walimueleza Balozi Seif kwamba nguzo zilizobeba waya hizo zimeanguka kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa.
Hata hivyo baadhi ya wakaazi wa eneo hilo wameamua kuzitumia waya hizo kwa kuanikia nguo zao jambo ambalo ni hatari kwa mujibu wa kanuni na taratibu za sekta ya umeme.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
22/3/2013.
Post a Comment