Dk. Shein: Tudumishe amani kukuza utalii

Wednesday, 13 March 20130 comments

RAIS wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, amesema sekta ya utalii ina nafasi kubwa ya kufanikisha mpango wa kuondoa tatizo la ajira na kukuza uchumi na kupunguza umaskini kwa wananchi wake.

 Dk. Shein ametoa tamko hilo jana katika kikao cha majumuhisho ya ziara yake ya Mkoa wa Kusini Unguja kilichofanyika huko Tunguu mjini Zanzibar jana. Alisema tatizo la ukosefu wa ajira linaweza kupatiwa ufumbuzi wa haraka kama wananchi wataanzisha miradi ya utalii katika maeneo yao na kutumia sekta hiyo kujiongezea kipato na kutangaza sekta ya utalii Zanzibar.

 Aidha, alisema Mkoa wa Kusini Unguja umebahatika kuwa ukanda wa utalii na kuwa na nyumba za kulala wageni 105 mbali na hoteli 37 za kitalii katika mkoa huo. “Vijana wengi wamepata ajira katika sekta ya utalii tangu kuanza kwa utekelezaji wa sera ya utalii kwa wote Zanzibar,” alisema Rais Dk. Shein.

 Alisema lengo la serikali yake ni kuona sekta ya utalii inaendelea kubakia kuwa sekta kiongozi kutokana na mchango wake mkubwa katika utekelezaji wa mpango wa kukuza uchumi na kupunguza umaskini kwa wananchi wake.

 Hata hivyo haliwataka viongozi wa mkoa huo kushirikiana na Kamisheni ya Utalii, yombo vya ulinzi na usalama na wenye mahoteli kumaliza vitendo vya uhalifu dhidi ya wageni. “Pamoja na taarifa ya kuimarika kwa hali ya ulinzi na usalama bado kuna taarifa za baadhi ya matukio ya uporaji wa watalii kwenye mkoa wenu,” alisema Rais Dk. Shein.

 Alisema kwamba lazima viongozi wa mkoa wahakikishe kuna kuwepo na jitihada za makusudi za kukabiliana na matukio hayo. Rais Shein alisema kwamba matukio ya uhalifu dhidi ya wageni yana madhara makubwa kwa maendeleo ya utalii na wananchi wake. Dk. Shein alisema kuwa takwimu zinaonesha katika kipindi cha Juni hadi Desemba 2012 makosa makubwa 686 yameripotiwa katika mkoa huo ingawa idadi hiyo ni ndogo ikilinganishwa na makosa 1,112 yaliyoripotiwa katika mwaka 2011.

Kuhusu sekta ya biashara, Dk. Shein alisema ni hatua muafaka kwa wananchi kuanzisha SACCOS na vikundi vya ushirika na kutumia soko la biashara la utalii katika ukanda huo. Sekta ya utalii Zanzibar imekuwa ikichangia asilimia 27 ya pato la taifa na asilimi 83 ya fedha za kigeni kutokana na watalii 170,000 wanaotembelea Zanzibar kila mwaka.

CHANZO TANZANIA DAIMA.
Share this article :

Post a Comment

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. Zanzibar News - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger