Kikao cha Kamati ya Taifa ya
Maadhimisho ya sherehe na Mapambo Zanzibar kimekutana kutathmini maadhimisho ya
Sherehe zilizopita za Kutimia miaka 49 ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Mwaka 1964
yaliyowakomboa Wakwezi na Wakulima wa Taifa hili.
Wajumbe wa Kikao hicho wakiwa chini
ya Mwenyekiti wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wamekutana
katika ukumbi wa nyuma wa Jumba la Wananchi Forodhani Mjini Zanzibar.
Akiwasilisha Taarifa ya Tathmini hiyo
Kaimu Katibu wa Sekriterieti ya Kamati hiyo ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Nd. Said Shaaban alisema kwamba Kamati zote zimetekeleza vyema majukumu yake
kama zilivyopangiwa.
Nd. Said aliwaeleza wajumbe hao kuwa
licha ya ufanisi huo lakini zipo baadhi ya changamoto zilizojichomoza ndani ya
utekelezaji wa kamati hizo ambazo alizitaja kuwa ni ufinyu wa Bajeti kulingana
na shughuli zilivyopangwa pamoja na ushiriki mdogo wa maafisa wa Serikali na
Masheha kwa dhana ya kwamba wao sio wahusika.
Nd. Said alisema katika kufanikisha
nusu karne ya Maadhimisho ya Sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar kutimia miaka 50
Sekriterieti imependekeza kutumiwa vyema vyombo vya Habari hasa vile vya
Serikali katika kushajiisha umma kuelewa umuhimu wao wa kushiriki vyema katika
maadhimisho hayo ya kihistoria.
Akitoa nasaha zake Mwenyekiti wa
Kamati hiyo ya Taifa ya Maadhimisho ya
Sherehe na Mapambo ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif
alizipongeza kamati zote kwa kufanikisha vyema sherehe za kutimia miaka 49 ya
Mapinduzi ya Zanzibar.
Balozi Seif alifahamisha kwamba
sherehe za miaka 49 zimefanikiwa vyema kutokana na ushirikiano mzuri uliopo baina
ya Viongozi, Wafanyakazi wa Taasisi za Umma na zile binafsi pamoja na Wananchi.
“ Wajumbe wakati tunaipokea Tathmini
hii ya sherehe za maadhimisho ya kutimia miaka 49 ya Mapinduzi ya Zanzibar
tunapaswa kuanza safari kubwa ya sherehe hizi kutimia miaka 50 ya Mapinduzi
yetu matukufu sawa na kusema Nusu Karne”. Alieleza Balozi Seif.
Wajumbe wa Kamati ya Taifa ya Maadhimisho
ya Sherehe na Mapambo wanatarajiwa kukutana tena katika kipindi cha mwezi mmoja
ujao kuendelea kupanga mikakati ya maandalizi ya maadhimishop hayo ya Nusu
Karne ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964.
Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais
wa Zanzibar Balozi Seif akakiongoza Kikao cha Kamati ya Maafa Zanzibar kujadili
namna ya Taifa linavyoweza kujiandaa dhidi ya maafa au matatizo yoyote yanayoweza kutokea katika kipindi hichi
cha mvua za masika zilizokwishaanza.
Kikao hicho kilichojumuisha wajumbe
wa kamati hiyo kutoka Unguja na Pemba kilifanyika katika ukumbi wa Ofisi ya
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar iliyopo Vuga Mjini Zanzibar.
Akiwasilisha Taarifa juu ya mwelekeo
wa Mvua za Masika mwezi wa Machi hadi Mei mwaka huu Mkurugenzi wa Idaya ya
Maafa Zanzibar Nd. Ali Juma Hamad alisema pamoja na kuwa na matarajio ya mvua
za wastani katika maeneo mengi, lakini bado upo uwezekano wa kutokea miripuko
ya magonjwa.
Ndugu Hamad alisema taasisi
zinazohusika na maafa zinapaswa kuchukuwa
hatua za tahadhari katika maandalizi ya kukabiliana na madhara
yanayoweza kusababishwa na Mvua za
masika za mwaka huu.
Akizungumzia sekta ya kilimo na
usalama wa chakula Nd. Hamad alisema maeneo mengi ya ukanda wa pwani ya
kaskazini pamoja na Visiwa vya Zanzibar yanatarajiwa kuwa na unyevu unyevu wa
kutosha wa udongo hali ambayo wakulima wanashauriwa kuendelea na taratibu za kawaida za Kilimo
cha msimu wa mvua za masika.
Akikiahirisha Kikao hicho Mwenyekiti
wa Kamati hiyo ya Maafa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliiagiza Idara ya Maafa
Zanzibar kwa kushirikiana na wataalamu wa Taasisi washirika kuandaa utaratibu
mahsusi wa kutoa taarifa rasmi kwa
Wananchi mapema wiki ijayo itakayosaidia Jamii kuwa na hadhari dhidi ya majanga
yoyote yanayoweza kutokea katika mvua za masika.
Balozi Seif alisema Serikali pamoja
na Jamii yote inapaswa kujitayarisha na hali yoyote ya majanga au maafa kulingana na msimu wa
masika uliokwishaanza mapema mwezi huu.
Wakichangia katika Kikao hicho baadhi
ya Wajumbe wa Kamati hiyo wamesema Wananchi walio wengi hadi sasa hawajawa na utamaduni ya kufuatilia mienendo ya mifumo ya hali ya hewa
nchini ambayo ni muhimu katika maisha yao ya kila siku.
Othan Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar
15/3/2013.
Post a Comment