Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Balozi Seif Ali Iddi amewakumbusha Madaktari Nchini kuzingatia maadili yao ya
kazi kama wanavyokula kiapo lengo likiwa kuwapa faraja na afuweni wagonjwa
wanakwenda Hospitalini na Vituo vya afya ili kupata huduma bora za afya.
Kumbusho hilo alilitoa wakati alipowatembelea na kuzungumza
nao Wanafunzi wa Fani ya Udaktari wanaopata mafunzo chini ya Madaktari mabingwa
kutoka Jamuhuri ya Watu wa Cuba hapo Hospitali kuu ya Mnazi Mmoja Mjini
Zanzibar.
Balozi Seif amesema Wagonjwa na hasa
Wananchi hujenga matumaini mazuri wakati wanapopata huduma safi, na hii
hupatikana iwapo madaktari husika
watakuwa wakizingatia zaidi taratibu zinazowaelekeza kutekeleza vyema majukumu
yao ya kila siku.
Amesema Serikali imelazimika kuwa na utaratibu
maalum wa kuwasomesha vijana wake katika fani ya Udaktari hapa Nchini kwa
matumaini ya kuwa na watendaji wa kutosha wa sekta hiyo watakaokidhi mahitaji
hapa Nchini.
“ Utafiti unaonyesha kwamba utaratibu
huu umeonyesha mwanga wa kupata idadi kubwa ya madaktari wazalendo mpango ambao
unapunguza wimbi la ukimbizi kwa vijana wetu wanaopata fursa ya kusoma vyuo vya
nje, akavitolea mfano vile vya ulaya na Bara la Asia kwamba wakimaliza mafunzo
yao wanaishia katika Nchi hizo kimaisha”. Alifafanua Balozi Seif.
Alifahamisha kwamba mpango huu
ulionzishwa kwa karibu miaka sita iliyopita ni mwanzo mzuri kwa Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar kuanzisha mafunzo
ya Sayansi ya Udaktari katika Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar { SUZA }.
Aliwataka wanafunzi hao kuhakikisha
kwamba lile lengo lililokusidiwa na
Serikali kupitia Wizara ya Afya ya kuwa na Madaktari zaidi wazalendo Nchini
wanalitekeleza vyema kwa kufanya kazi kwa bidii mara wamalizapo mafunzo yao.
Balozi Seif alielezea matumaini yake
kwamba wanafunzi hao watatekeleza majukumu yao wakielewa kwamba watu
wanaowahudumia ni miongoni mwa ngugu, wazee na jamaa zao waliowazunguuka.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
aliwapongeza walimu wa wanafunzi hao Kutoka Jamuhuri ya Watu wa Cuba kwa umahiri wao wa kusaidia kuwafinyanga
vyema wanafunzi hao wa fani ya Udaktari Zanzibar.
Mapema wakielezea changamoto
zinazowakabili chuoni hapo baadhi ya Wanafunzi hao walisema ufinyu wa posho sambamba
na ucheleweshwaji wake ni moja ya tatizo lililokuwa likiwapa usumbufu mkubwa
wakati katika mafunzo yao.
Walizitaja changamoto nyengine kuwa
ni pamoja na kupatiwa fursa za masomo ya juu hapo baadaye iwe ndani au nje ya Nchi pamoja na migongano baina yao
na baadhi ya wafanyakazi wa Hospitali Kuu ya Mnazi mmoja wakati wanapokuwa
katika mazoezi ya vitendo.
Akitoa ufafanuzi wa hoja hizo Katibu
Mkuu Wizara ya Afya Dr. Saleh Mohammed Jidawi alisema asilimia kubwa ya
changamoto hizo zimo ndani ya uwezo wa Wizara husika ambapo aliwawakikishia
kwamba Uongozi wa Wizara utazifanyia
kazi kadri hali inavyoruhusu.
Dr. Jidawi alisema ni fahari kwa
Uongozi na wafanyakazi wa Wizara ya Afya kuona kwamba Wanafunzi hao
wanafanikiwa vyema katika maisha yao ya kazi hapo baadae kwani kwa mujibu wa
fani yao wao ni miongoni mwa sehemu ya Wizara hiyo.
Wanafunzi hao 50 ambao kati yao 38
kutoka Unguja na 21 kutoka Kisiwani Pemba wanatarajiwa kumaliza mafunzo yao ya
miaka Sita ya Udaktari katika daraja
la Udaktari { yaani Medical Doctor - M.D
} ifikapo mwezi Julai mwaka huu wa 2013.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar
16/3/2013.
Post a Comment